Natowa kitandawili / mwenye jawabu kutowa
Wako watu sura mbili / majaraha yasopowa
Kuchupa kwao kuwili / nyoyo zao zaunguwa
Watakayo ni muhali / milele hayatokuwa.
Akili zao ni ghali / kutu zinawasumbuwa
Wapigana na makali / mwenye fani hupekuwa
Warejea ya awali / hawavuki zao puwa
Wala hawana muhali / wamegeuka viluwa.
Wanapeta pili pili / ungó wao chandaruwa
Upungufu wa akili / ukweli kuutambuwa
Wasemavyo waawali / wengine wajisumbuwa
Hatari yawakabili / kuviwasha vilopowa.
Mkahawa sihoteli / kushindana kutambuwa
Dibeti zisoukweli / mtuno wakitumbuwa
Kisu kutiwa makali / mwerevu anang´amuwa
Ukweli muukubali / mwiko mwenziwe upawa.